MASWALI NA MAJIBU 

MADA: Kwa nini Watumishi wa Serikali za Mitaa wajiunge na TALGWU?

 1. TALGWU ni nini?

Ni Chama cha wafanyakazi wa serikali za Mitaa Tanzania ambacho kimesajiliwa chini ya sheria ya vyama vya wafanyakazi no 10 ya mwaka 1998, na kilipewa nambari ya usajili  010 tarehe 15/09/2000.

TALGWU inaunganisha wafanyakazi wote waliopo chini ya Mamlaka za serikali za mitaa na Taasisi nyingine  nchini ambapo hadi kufikia June 2018, Chama kilikuwa na wanachama 62,170.

TALGWU inajishirikisha na shirikisho la vyama vya wafanyakazi Tanzania (TUCTA) ,shirikisho la vyama vya wafanyakazi vinavyotoa huduma kwa umma duniani (PSI) na Mtandao wa Vyama vya Wafanyakazi vya Serikali za Mitaa  Africa (AMALGUN).

Hivyo basi chama cha wafanyakazi ni ummoja, muungano, na mshikamano wa wafanyakazi ambao nia, malengo, matakwa na matarajio yao yanafanana.

Umoja huo ndio nguzo pekee ya kupatia ufumbuzi wa matatizo yao.

TALGWU inaelimisha, inatetea, na kulinda ajira na ujira wa wanachama wake kwa kuzingatia sheria, taratibu, kanuni, miongozo na nyaraka mbalimbali za kazi.

 1. Je madhumuni ya kuanzishwa TALGWU ni yapi?

 • Kupigania na kuwahimiza waajiri kuboresha na kuendeleza hali nzuri ya wanachama katika maisha yao wakiwa kazini na wakati wa kustaafu.
 • Kujadiliana na kuondoa tofauti zinazojitokeza kati ya waajiri na wanachama, au mwanachama mmoja na mwingine kwa njia ya majadiliano/makubaliano ya amani kila itakapowezekana.
 • Kusimamia na kushauri katika uundaji wa mikataba ya hari bora mahali pa kazi.
 • Kuwaelimisha wanachama katika kuelewa sheria, kanuni na taratibu za nidhamu zinazotumika nchini.
 • Kuwasiliana na serikali kuhusu haja ya kutunga sheria sahihi za kazi na kuandaa sera nzuri za kuendeleza uchumi na maisha ya jamii.
 • Kulinda maslahi ya wanachama kwa kuwasiliana na serikali ili kuepukana na uandaaji wa sera ambazo ni hatari kwa wanachama.
 • Kuishauri Serikali kupunguza kodi ya mishahara ya mfanyakazi.
 • Kuishauri Serikali kurekebisha na kutengeneza Miundo ya Utumishi wa Umma ambayo haiwaumizi Wanachama wetu
 1. Kwanini wafanyakazi wa Serikali za Mitaa wajiunge na TALGWU?

 • Ili kuwa na umoja katika kupigania haki na maslahi yao.
 • Kupata uwakilishi katika vyombo vya maamuzi.
 • Kupata msaada wa kisheria pale wanapokumbwa na migogoro kazini.
 • Kuelimishwa kuhusu masuala mbalimbali ya kiutumishi.
 1. Ni changamoto zipi zinaikabili TALGWU katikakutekeleza majukumu yake kama Chama cha Wafanyakazi?

 • Madai ya haki za msingi ya Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa wasio waalimu.
 • Kutopandishwa madaraja kwa wakati
 • Mabaraza ya Wafanyakazi kutofanyika kwa mujibu wa sheria
 • Pamoja na agizo la Serikali la kuwarejesha kazini Watumishi walioondolewa kazini kwa cheti cha darasa la saba lakini kuna baadhi ya Waajiri bado hawajatekeleza agizo hilo. Aidha Wanachama hao waliorejeshwa bado hawajalipwa mishahara yao ya kipindi wamesimamishwa kazi.
 • Watumishi wanaolipwa kwa mapato ya ndani kucheleweshewa kupata mshahara na makato yao ya kisheria kutopelekwa kwa wakati kwenye taasisi husika na kupelekea kukosa baadhi ya huduma kama vile matibabu na mikopo.
 • Wanachama wetu kudhalilishwa kutokana na matumizi mabaya ya madaraka kwa baadi ya wanasiasa ambapo huwachukulia hatua wanachama wetu bila kuzingatia kwamba wao sio mamlaka zao za nidhamu .
 • Baadhi ya waajiri kuwafukuza kazi wanachama wetu bila kufuata kanuni, sheria na taratibu za nchi.

 

 1. JE TALGWU INA MPANGO MKAKATI GANI  KATIKA KUHAKIKISHA INATOA HUDUMA BORA KWA WANACHAMA WAKE?(mpango mkakati 2018 – 2022

 2. 1 Kulinda na kuoanisha mazingira na hali bora ya kazi kwa Wafanyakazi wote wa Mamlaka za Serikali za Mitaa. Pamoja na mafanikio ambayo Chama kimepata kipindi kilichopita, lakini ukweli ni kwamba kiwango cha mishahara ya Wafanyakazi ambao ni Wanachama wetu bado haikidhi hivyo TALGWU itajikita katika tafiti zenye lengo la kubaini uwiano wa mishahara kati ya Watumishi wa Serikali za Mitaa na sekta nyingine ili kupata msingi wa majadiliano na Mwajiri, kujenga misingi ya majadiliano ya pamoja na Serikali juu ya mishahara bora kwa Wafanyakazi, kuanzisha programu ya kufadhili Wanachama wanaojiunga na elimu ya juu pamoja na kumshawishi Mwajiri kuboresha Ofisi wanazotumia Wanachama wetu na kutoa vitendea kazi.
 1. Kukifanya Chama kuwa msemaji mkuu kwa niaba ya Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa kutoka ngazi ya Taifa hadi chini ambapo Chama kitaongeza idadi Wanachama kutoka 67% ya wafanyakazi wote wa Serikali za Mitaa kwa sasa hadi 95% ya wafanyakazi wote wa Serikali za Mitaa ifikapo mwaka 2022 pamoja na kufikia kuwa na mbinu ya pamoja katika kushughulikia masuala yote yanayoathiri utoaji wa huduma bora kwa Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa kwa kipindi chote cha uhai wa mpango mkakati huu.
 1. Kuendeleza ustawi wa kusimamia maslahi ya Wanachama katika vifungu ambavyo vitaruhusu ustawi wao wa kitaaluma na kiuchumi ambapo Chama kitalinda na kutetea maslahi ya Wanachama wetu katika kipindi chote cha utekelezaji wa mpango mkakati huu, kuendelea kuifadhili TALGWU MICROFINANCE PLC ili iweze kukopesha Wanachama wengi zaidi pamoja na kudumisha hadhi ya ustawi wa kiuchumi na kijamii ya Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa kwa kipindi chote cha uhai wa mpango mkakati huu.
 1. Kuanzisha na kudumisha uhusiano na ushirikiano na wadau wengine ambapo Chama kitaendelea kuimarisha uhusiano uliopo kati yake na Vyama vingine vya Wafanyakazi na wadau mbalimbali ndani ya nchi, Kikanda na Kimataifa pamoja na kuendeleza na kudumisha mahusiano na mashirikiano mengine kwa maslahi ya Wanachama wetu katika kipindi chote cha utekelezaji wa mpango.
 1. Kujenga na kuboresha uwezo wa kitaasisi wa Chama. Katika kutekeleza hili, Chama kimejipanga kuongeza wigo wa ukusanyaji mapato, kuboresha usimamizi wa kimenejimenti na kiuongozi, kutoa msaada wa miundombinu utakao kiwezesha Chama kutekeleza shughuli zake za msingi ipasavyo, kuendeleza juhudi za kuwepo kwa usawa wa jinsikwenye ngazi zote za uongozi wa Chama pamoja na kuinua TALGWU Makao makuu kufikia hadhi ya viwango vya Kimataifa ifikapo 2022.

Hivyo basi kutokana na maeneo matano yaliyoelezewa hapo juu ambayo kama Chama tumejiwekea katika mpango mkakati kwa mwaka 2018 – 2022, tunatarajia pia kutekeleza masuala yafuatayo ili kuwa na TALGWU imara, bora na yenye nguvu katika kulinda, kusimamia na kutetea haki, maslahi na hadhi ya Wanachama wetu:

 • Kuwezesha Matawi kufanya shughuli za Chama kwa mujibu wa Katiba kwa Kupeleka Fedha za masurufu kwa wakati na kwa kiwango sahihi kila mwezi.
 • Chama kitaongezajuhudi katika Kuishauri Serikali kutoa miundo iliyoboreshwa/ mipya ya Utumishi wa Umma ambayo sio kandamizi. Na itakayo toa motisha kwa Wafanyakazi kuongeza juhudi katika kazi.
 • Tumeandaa utaratibu mzuri wa Kutoa mafunzo kwa Viongozi wa Matawi mpaka Taifa ili wajue majukumu yao na kuwaongezea uwezo katika kushughulikia masuala mbalimbali ya Wafanyakazi. lengo likiwa ni kuwajengea uwezo katika kutatua kero na matatizo ya Wafanyakazi katika maeneo ya kazi.
 • Chama kimejiandaa Kufanya ziara za mara kwa mara ili kujua kero na changamoto mbalimbali zinazowakabili Wanachama wetu na kutafuta namna bora na ya haraka ya kukabiliana nazo. Hii itapelekea Wanachama kukielewa zaidi Chama na hivyo kushiriki kikamilifu katika shughuli mbalimbali za Chama.
 • Kuhakikisha madai ya haki za msingi za Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa yanalipwa yote. Hii ni kero ya muda mrefu ambayo Chama kinaona haina sababu kuendelea kuwepo kwa sababu inapunguza morali ya Wafanyakazi na jitihada mbalimbali zinaendelea ikiwemo majadiliano ya pamoja na Serikali.Vilevile Chama kitatengeneza mfumo bora wa mawasiliano kutoka Matawini hadi Taifa. Chama kimekusudia kurahisisha upatikanaji wa taarifa za masuala mbalimbali yaliyoamuliwa katika ngazi zote kwa kuweka mfumo ambao taarifa zitafika kwa haraka .
 • Kuendelea kutoa matamko na taarifa mbalimbali za Chama kupitia vyombo vya Habari, Chama kimedhamiria kuikumbusha Serikali juu ya mambo mbalimbali ambayo yanawakwaza wafanyakazi ili yaweze kupatiwa ufumbuzi kwa haraka na wakudumu kwa masuala kama vile ucheleweshwaji wa haki mbalimbali, sheria mbaya, Wanasiasa kuingilia utendaji na matumizi yao mabaya ya madaraka.
 • Kuwaunganisha wanachama wote kuwa kitu kimoja katika kushughulikia masuala ya watumishi kwani umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu. TALGWU inaamini katika umoja kama ndio silaha pekee ya kumkomboa mfanyakazi ndiyo sababu mara kwa mara inahubiri umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu.
 • Aidha Chama kitajenga na kuhimiza misingi ya uwajibikaji kwa Wanachama wake. Kwa kuwa uwajibikaji ni moja ya masuala ambayo Vyama vya Wafanyakazi vinapaswa kuhimiza Wanachama wake, TALGWU nayo kwa ngazi zote inayo wajibu wa kuwakumbusha Wanachama kuwajibika kikamilifu katika maeneo yao ya kazi tukiamini kuwa haki bila wajibu ni kazi bure.
 • Kukimarisha Chama kiuchumi ili kutoa huduma stahiki kwa wanachama. Ikumbukwe kuwa Uchumi ni nguzo muhimu katika kutoa huduma. Chama kikiwa na uchumi mzuri na imara, bila shaka uwezo wake wa kutoa huduma kwa Wanachama utakuwa ni wa uhakika. Kwa maana hiyo TALGWU itahakikisha inatunza na kuendeleza vitega uchumi vilivyopo ili kuwa na Chama imara na chenye nguvu.